MWANAMUZIKI mkubwa barani Afrika aliyekuwa akiunda Kundi la P Square kutoka Nigeria, Peter Okoye ‘Mr P’ anateseka baada ya kukutwa na Virusi vya Corona vinavyosababisha Ugonjwa wa COVID -19.
Kwa mujibu wa Mr P, yeye, mkewe pamoja na binti yao walipatikana na Corona wiki tatu zilizopita. Mr P anasema, yeye na familia yake wanapitia wakati mgumu mno ila anamshukuru Mwenyezi Mungu wapo hai.
Mbali na yeye, mkewe na mtoto wao, pia wafanyakazi wake wawili wa nyumbani nao walikutwa na virusi hivyo mapema mwezi uliopita.
“Kwa muda wa wiki tatu zilizopita, nimepitia wakati mgumu na wengi hamkujua kwa nini nilikuwa kimya, nilisema iwe siri kwangu, nimekuwa na Virusi vya COVID -19, mke wangu pia alipatikana na virusi hivyo,” amesema Mr P.
Ameongeza kuwa, mkewe Lola na mwanawe walipatikana na virusi hivyo na kwa sasa wamewekwa karantini.
“Nilikuwa mgonjwa sana na nikawekwa karantini, nisingeweza kumuona binti yangu mgonjwa, nilijisikia vibaya sana, najutia sana kuwaletea familia yangu ugonjwa huu hatari,” anasema Mr P akikiri kwamba, yeye ndiye alileta virusi hivyo nyumbani kutoka kwenye mizunguko yake duniani.
Mr P na pacha wake Paul walikuwa wakiunda Kundi la P-Square ambalo lilivunjika miaka kadhaa iliyopita kutokana na kutoelewana kwenye mgawanyo wa mapato.
EmoticonEmoticon