HISIA za mapenzi hutokea ndani kabisa ya moyo. Kila mmoja ana uhuru na haki ya kupenda. Huwezi kuchaguliwa wa kumpenda! Mapenzi ni maisha ya mtu katika uhalisia wake.
Maana yake ni kwamba kama utakuwa na mtu ambaye moyo wako hauna mapendo ya dhati kwake, tafsiri yake ni kwamba maisha yako yote yatakuwa yenye mateso kila siku.
Utalala na mtu usiyempenda, utaamka naye na utaambatana naye baadhi ya sehemu wakati moyo wako haukuwa tayari kuwa naye.
Hilo ni tatizo. Kwa bahati mbaya kuna baadhi ya wazazi bado wana mawazo na fikra za kizamani. Wapo wanaoendelea kuwachagulia au kuwalazimisha watoto wao wenzi wa kuishi nao. Ndugu zangu, hizo ni zama za kale. Maisha yamebadilika. Kila kitu kimebadilika. Ni sahihi zaidi mtu achague mwenzi wa maisha yake mwenyewe maana ataishi naye yeye.
Huo ni upande mmoja; upande mwingine ni haki ya mwanamke kupenda. Imezoeleka mwanaume ndiye mwenye mamlaka ya kumpenda mwanamke na kumtaka waanzishe uhusiano. Inategemea kama mwanamke atakubali au atakaa. Pengine ni utaratibu sahihi maana ni uamuzi wa mwanamke na kuangalia moyo wake kama ni kweli amempenda mwanaume huyo au lah kisha anaamua mwenyewe.
Kuna wakati mwanamke anazama mapenzi kwa mwanaume. Kila akipita mbele yake moyo unalipuka. Kila anachokifanya anazuzuka. Mapenzi yamemwingia lakini ‘sheria’ inambana. Hawezi kuanzisha uhusiano yeye. Hata kama akiamua kujipeleka, mwisho wao hauwi mzuri – wataachana tu (mara nyingi). Tafiti zinaonyesha kuwa, uhusiano ulioanzishwa na mwanamke mara nyingi huwa hauna mafanikio kama unaoanzishwa na mwanaume.
Akili za wanaume wengi huamini mwanamke anapomfuata na kumtaka kimapenzi ni mhuni au kwa lugha za vijana anaonekana hajatulia! Si jambo sahihi, hutegemea na moyo wa mhusika na namna anavyoonesha mapenzi yake lakini ndivyo ilivyozoeleka.
Pamoja na hayo, mwanamke anaweza kumvutia mwanaume aliyempenda na kumuingiza kwenye himaya yake kwa kufuata utaratibu ulio sahihi na penzi likadumu. Yapo mambo ya msingi ya kuzingatia katika harakati hizo.
Kwanza kabisa kama mwanamke unapaswa kuwa katika mwonekano mzuri wa kike wenye kuvutia muda wote. Hapa nasema hivyo kwa sababu, wapo wanawake ambao wanahangaika na hawajaolewa au hawajapata watu ‘waliotangaza nia’ kwa sababu tu hawajiweki katika mwonekano mzuri. Mwanamke jitambue. Tengeneza na hifadhi mvuto wako siku zote. Zingatia mavazi bora yenye staha na kukusitiri. Mtindo wa nywele na vipodozi vinginevyo kulingana na mahali ulipo.
NINI CHA KUFANYA?
Kwanza ni lazima uvutie, lakini sasa hapa tunakwenda mbele zaidi. Umeshamuona mwanaume ambaye ni chaguo lako na kwa bahati mbaya hana ‘time’ na wewe. Uteseke moyoni? Hapana. Vipo vitu ambavyo ukivifuata, utamsogeza mwanaume huyo na mwisho atakuwa wako. Huna sababu ya kubaki na jakamoyo. Silaha ya kwanza kabisa ni kumjua vizuri huyo mwanaume.
Anaishi wapi? Anafanya wapi kazi nk. Inawezekana ikawa vigumu kidogo kujua kila kitu kwa wakati mmoja lakini angalau ukijua kimojawapo itakuwa sawa, usipojua itakuwa imekula kwako! Mathalani mnafanya naye kazi au huwa anakuja ofisini kwako/kwenu, mnakutana kwenye mikutano au mnaishi mtaa mmoja nk. Hayo ni mambo ya muhimu kuyajua ili uweze kumweka katika mtego wako.
Mvute kwako. Si kwa kumwambia lakini hata kwa vitendo tu. Vaa mavazi mazuri (naomba kusisitiza hapa mavazi ya heshima) ambayo hayatakutafsirisha kama mwanamke asiye na staha. Wanaume wengi wanapenda kuwa na wanawake wenye staha na wanaotambua heshima yao. Ukijidanganya na kuvaa mavazi ya kujiachia mwili wako, maana yake atakuchukulia kama mwanamke ambaye hujatulia.
Wakati unajaribu kumvutia kwako pia chunguza vitu anavyopenda. Utaweza kujua kwa kumfuatilia hata kwa kidogo tu. Ukigundua angalau mtindo mmoja anaoupenda, mtege nao. Tafuta mbunifu ambaye atakuweka katika mtindo ambao anavutika nao.
Kumbuka ni sumu kumfuata mwanaume na kumwambia kuwa unampenda. Kamwe usianzishe uhusiano wewe.
EmoticonEmoticon