ZAMANI watu walizoea zaidi kuona komedi zikichezwa na wanaume, lakini baadaye wakaibuka wachekeshaji wa kike.
Miongoni mwa wachekeshaji walioibuka na kufanya vizuri ni pamoja na Salma Jabu ‘Nisha’, ambaye amepata umaarufu mkubwa kutokana na staili yake ya uigizaji na kuweza kugusa hisia za mashabiki tangu enzi za uhai wa nguli, Amri Athumani ‘Mzee King Majuto’.
Mwanamama huyu ameweza kucheza muvi kali kama vile Kiboko Kabisa, Zena na Betina, Gumzo, Tikisa, Hakuna Matata, Mtaa kwa Mtaa, Pusi na Paku na nyingine kibao.
RISASI limefanya naye mahojiano maalum (exclusive interview) ambapo amefunguka mengi ikiwemo ku-miss uwepo wa Mzee Majuto. Karibu:
RISASI: Umekuwa kimya sana kwenye kutoa kazi tatizo nini?
NISHA: Unajua tangu amefariki Mzee Majuto kwa kweli bado sijakaa sawa, kwa sababu nimepoteza mtu ambaye nilikuwa nikifanya naye kazi kwa muda mrefu na hapa tunavyoongea ndani nina script nyingi ambazo zilikuwa zikimuhusu yeye na mimi pamoja na watu wengine.
Kwa hiyo kutengua vile vitu kidogo imeniwiya vigumu na bado akili yangu haijakaa sawa kuingia kwenye gemu, kila nikitaka kufanya kuna vitu ambavyo naona vinajirudia kwangu.
Ndiyo maana kwa sasa hivi nimeamua kujipa muda kwanza nifanye mambo yangu ya biashara ila mambo yakikaa sawa nitafanya.
RISASI: Mzee Majuto ana msada gani kwenye sanaa yako?
NISHA: Ana mchango mkubwa sana, kwa sababu hakuwa tu msanii bali alikuwa kama mwalimu wangu, baba yangu, rafiki yangu na kwa bahati nzuri watu walikuwa wanapenda jinsi tulivyokuwa tunaigiza naye yani kifupi alikuwa ni kila kitu kwangu.
RISASI: Kitu gani ambacho alikuwa anakusihi sana kuhusiana na mambo yako ya sanaa?
NISHA: Kikubwa alikuwa akiniambia nisikate tamaa, na pia niangalie kitu gani ambacho kipo bora nifanye nisisikilize maneno ya watu, na pale ambapo nilikuwa sifanyi vizuri alikuwa ananirekebisha.
RISASI: Majuto ameacha pengo gani kwenye sanaa hususani kwa upande wako?
NISHA: Kaacha pengo kubwa sana, ndiyo maana mpaka leo nimeshindwa kusimama, nimejipa muda wa kujipanga tena.
RISASI: Tukirudi kwako mashabiki wangependa kufahamu Nisha ni mtu wa aina gani?
NISHA: Ni mama wa mtoto mmoja wa kike, naipenda familia yangu nawapenda watu wote wanaonipenda na wasiyonipenda, napenda sana kufanya kazi.
RISASI: Mwanao ana umri gani?
NISHA: Ana miaka 16.
RISASI: Mwanao anazungumziaje kipaji chako cha uigizaji?
NISHA: Ananipa sapoti sana na pia anakichukulia vizuri kwa sababu na yeye anapenda uigizaji.
RISASI: Kuna kipindi na yeye aliingia kwenye mambo ya uigizaji lakini kwa sasa amepotea tatizo nini?
NISHA: Ni kweli alikuwa akiigiza ila kwa sasa nimeamua kumstopisha kwanza ila awe bize na masomo.
RISASI: Unaishi na baba yake au wewe ni single mama?
NISHA: Hapana siishi naye kabisa nakaa na mwanangu.
RISASI: Unaizungumziaje Bongo Muvi ya sasa ukilinganisha na ile ya kipindi cha nyuma?
NISHA: Naona Bongo Muvi ya sasa hivi ni nzuri zaidi na wasanii wanajua wanachokifanya.
RISASI: Tunaona kuwa mambo yamebadilika, mastaa wengi sasa hivi wameamua kutunga tamthiliya zao wenyewewe, je tutegemee kitu gani kutoka kwako?
NISHA: Ndiyo hapa nilipo naandaa tamthiliya yangu na kila siku lazima niangalie muvi ili kujua mambo mapya yanayoendelea duniani.
RISASI: Ni lini utatambulisha rasmi kazi yako.
NISHA: Mwaka huu tupo kwenye production, Inshaallah mwakani ndiyo mwaka wa kuwapa watu kazi.
RISASI: Mahusiano yako na Snura yakoje kwa sasa, bado ni marafiki kama mwanzo?
NISHA: Yapo kama yalivyokuwa mwanzo, ila hatujawahi kuwa marafiki.
RISASI: Kuna kipindi hapo nyuma mambo yalisambaa kuwa Snura kakuibia bwana ambaye ni Minu, je kuna ukweli wowote?
NISHA: Hata kama kaniibia bwana ambaye nilishawahi kuwa naye mimi sipaswi kukasirika hata kidogo, kwa sababu ndiyo maisha ambayo yeye amechagua.
RISASI: Ni kweli kwamba ulikuwa unamlea Minu?
NISHA: (Anacheka) muulizeni mwenyewe Minu.
RISASI: Minu alishawahi kukutafuta na kukuomba msamaha wa kutaka mrudiane?
NISHA: Hatuwezi kurudiana lakini tulishawahi kuongea kawaida tu kusalimiana, unajua hata kama mmeachana isiwe ndiyo njia ya kutengeneza uadui, kama watu mlishawahi kupendana hapo awali haina haja ya kununiana.
RISASI: Upo kwenye uhusiano sasa hivi?
NISHA: Hapana kwa sasa nimeamua kupumzika kwanza, nimeamua kukita maisha yangu kwenye biashara.
RISASI: Kwa nini umeamua kuficha mahusiano yako Nisha.
NISHA: Hapana siyo kama naficha ila kiukweli sina mtu.
RISASI VIBES: Sasa hivi kumekuwa na kasumba inayosumbua wasanii wa kike kutoka na watoto wadogo, kwa upande wako unahisi sababu ni nini haswa?
NISHA: Hapo naomba nijizungumzie mimi kama mimi, kwanza huwa siangalii umri, unajua kuna kitu kinaitwa love(mapenzi).
Unakutana na mtu kwa mara ya kwanza ukatokea kumpenda mambo ya umri yatakuja baadaye, halafu watu wajue kwamba tabia ndiyo zinafanya watu wanaachana na siyo umri.
EmoticonEmoticon