Sunday, September 20, 2020

SIMBA: “Tumerudi Nyumbani Kuanza Kuwakera.”

Tags

 


SIMBA wanasema: “Tumerudi nyumbani kuanza kuwakera.” Hiyo ni baada ya kucheza mechi mbili nje ya Dar katika Ligi Kuu Bara msimu huu na kukusanya pointi nne.


 


Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara ambao leo watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar kupambana na Biashara United, katika mechi mbili za ugenini, ilianza kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu, mechi iliyochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya.




Baada ya hapo, ikalazimishwa sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro. Kwa upande wa Biashara, inaingia uwanjani leo ikiwa na ushindi wa asilimia 100 kutokana na kushinda mechi zote mbili nyumbani kwenye Uwanja wa Karume, Mara kwa matokeo ya 1-0 dhidi ya Gwambina na Mwadui.


 


Simba ikiwa imeruhusu mabao mawili kwenye mechi mbili, leo ina kazi kubwa ya kuipenya ngome ya Biashara ambayo katika mechi hizo, haijaruhusu bao.


 


Katika hilo, Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck, amewakabidhi majukumu mazito mawinga wake, Bernard Morrison na Luis Miquissone ya kuhakikisha wanaipenya ngome ya Biashara na kupata ushindi.Sven katika mazoezi ya mwisho kabla ya leo kucheza na Biashara, alikuwa akiwapatia mbinu za umaliziaji na kupiga mashuti nje ya 18 wachezaji wake wote ambapo mawinga hao walifanya kwa ustadi mkubwa.




Kocha wa Biashara United, Francis Baraza raia wa Kenya, amesema: “Tunaifahamu Simba ni timu kubwa, tangu msimu uliopita walikuwa na kikosi bora na msimu huu pia wamefanya usajili kwa kuwaongeza wachezaji wengine bora, hivyo natarajia tutakuwa na mchezo mzuri na mgumu.


 


“Licha ya kuwapa heshima kutokana na ukweli kwamba wao ndiyo mabingwa watetezi, lakini hatutawaogopa, tutajitahidi kucheza tukiwa na lengo la kusaka pointi tatu kwa kuwa tunao uwezo huo.”


 


REKODI


Huu ukiwa ni msimu wa tatu kwa Biashara United ndani ya Ligi Kuu Bara, imekutana na Simba mara nne.Katika mechi hizo, Simba imeshinda tatu na sare moja.


 


Haijapoteza, huku Biashara ikishindwa kupata ushindi mbele ya Simba.Mbali ya kushindwa kupata ushindi mbele ya Simba, pia Biashara haijaambulia ushindi wowote ilipotua Dar kucheza mechi ya ligi ikiwa imecheza Dar mara tisa. Ushindi wao mkubwa ni sare ambapo imezipata tatu na kupoteza mechi sita.


EmoticonEmoticon