KIUNGO mshambuliaji wa Yanga raia wa Angola, Carlos Fernandes ‘Carlinhos’, sasa hivi rasmi amehamishiwa pembeni namba 11 atakayokuwa anaicheza katika michezo ijayo ya Ligi Kuu Bara na mashindano mengine.
Muangola huyo alijiunga na Yanga msimu huu akitokea Interclube inayoshiriki Ligi Kuu ya Angola akisaini mkataba wa miaka miwili.
Kiungo huyo mwenye uwezo wa kupiga faulo, kona na mashuti ya mbali, amefanikiwa kutoa asisti mbili katika michezo mitatu ya Ligi Kuu Bara aliyocheza msimu huu.Akizungumza na Spoti Xtra, Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema kuwa kiungo huyo hivi sasa wamemuhamishia kucheza namba 11 na siyo 10 aliyokuwa akicheza awali.
Mwambusi alisema kuwa walianza kumuhamishia nafasi hiyo katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar na lengo la kumpeleka huko ni kumpa uhuru wa kucheza.
Aliongeza kuwa, awali walimtumia katikati kwenye michezo miwili na kuona mabeki wakimpania kwa kumchezea rafu za makusudi, hivyo haraka wakaamua kumpeleka pembeni ili awe huru zaidi kucheza.
“Kumtumia Carlinhos pembeni ilikuwa ‘game plan’ yetu, ni mchezaji mzuri ambaye ‘touching’ zake huwa na madhara kwa wapinzani, hivyo tulilazimika kumweka pembeni ili apate nafasi ya kucheza bila kusumbuliwa.
“Mechi dhidi ya Mtibwa, game plan yetu hiyo ilifanikiwa ambapo alitengeneza nafasi kadhaa za kufunga, alipiga kona tano na moja kati ya hizo, ilizaa bao lililofungwa na Moro (Lamine), hivyo Carlinhos ni mchezaji mmoja hatari mwenye madhara ambaye lazima awepo katika timu,” alisema Mwambusi.
EmoticonEmoticon